‏ Ezekiel 25

Unabii Dhidi Ya Amoni

1Neno la Bwana likanijia kusema: 2 a“Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Waamoni utabiri dhidi yao. 3 bWaambie, ‘Sikieni neno la Bwana Mwenyezi. Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kwa sababu ulisema, “Aha!” juu ya mahali pangu patakatifu palipotiwa unajisi, na juu ya nchi ya Israeli ilipoangamizwa, na juu ya watu wa Yuda walipokwenda uhamishoni, 4 ckwa hiyo nitawatia mikononi mwa watu wa mashariki mkawe mali yao. Watapiga kambi zao katikati yenu na kufanya makazi miongoni mwenu, watakula matunda yenu na kunywa maziwa yenu. 5 dNitaufanya mji wa Raba kuwa malisho ya ngamia na Amoni kuwa mahali pa kondoo pa kupumzikia. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana. 6 eKwa kuwa hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kwa kuwa umepiga makofi yako na kufanya kishindo kwa miguu, mkifurahia kwa mioyo yenu miovu juu ya yale mabaya yaliyoipata nchi ya Israeli, 7 fhivyo nitaunyoosha mkono wangu dhidi yako na kukutoa kuwa nyara kwa mataifa. Nitakukatilia mbali kutoka kwenye mataifa na kukungʼoa katika nchi. Nitakuangamiza, nawe utajua ya kuwa Mimi ndimi Bwana.’ ”

Unabii Dhidi Ya Moabu

8 g“Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: ‘Kwa sababu Moabu na Seiri wamesema, “Tazama, nyumba ya Yuda imekuwa kama mataifa mengine yote,” 9 hkwa hiyo nitaiondoa ile miji iliyo kando ya Moabu, kuanzia miji iliyoko mipakani, yaani: Beth-Yeshimothi, Baal-Meoni na Kiriathaimu, iliyo utukufu wa nchi hiyo. 10 iNitaitia Moabu pamoja na Waamoni mikononi mwa watu wa Mashariki kuwa milki yao, ili kwamba Waamoni wasikumbukwe miongoni mwa mataifa, 11 jnami nitatoa adhabu kwa Moabu. Ndipo watakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana.’ ”

Unabii Dhidi Ya Edomu

12 k“Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: ‘Kwa sababu Edomu ulilipiza kisasi juu ya nyumba ya Yuda na kukosa sana kwa kufanya hivyo, 13 lkwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Nitaunyoosha mkono wangu dhidi ya Edomu na kuua watu wake na wanyama wao. Nitaufanya ukiwa, kuanzia Temani hadi Dedani wataanguka kwa upanga. 14 mNitalipiza Edomu kisasi kwa mkono wa watu wangu Israeli, nao watawatendea Edomu sawasawa na hasira yangu na ghadhabu yangu, nao watakijua kisasi changu, asema Bwana Mwenyezi.’ ”

Unabii Dhidi Ya Ufilisti

15 n“Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: ‘Kwa sababu Wafilisti wamewalipiza kisasi kwa uovu wa mioyo yao na kwa uadui wa siku nyingi wakataka kuangamiza Yuda, 16 okwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Mimi ninakaribia kuunyoosha mkono wangu dhidi ya Wafilisti, nami nitawakatilia mbali Wakerethi na kuwaangamiza wale waliosalia katika pwani. 17 pNitalipiza kisasi kikubwa juu yao na kuwaadhibu katika ghadhabu yangu. Ndipo watakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana, nitakapolipiza kisasi juu yao.’ ”

Copyright information for SwhNEN