‏ Exodus 16

Mana Na Kware

1 aJumuiya yote ya Kiisraeli ikaondoka Elimu, wakafika Jangwa la Sini, lililokuwa kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka Misri. 2 bHuko jangwani hiyo jumuiya yote wakawanungʼunikia Mose na Aroni. 3 cWaisraeli wakawaambia, “Laiti tungelikufa kwa mkono wa Bwana huko Misri! Huko tuliketi tukizunguka masufuria ya nyama na tukala vyakula tulivyovitaka, lakini ninyi mmetuleta huku jangwani ili mpate kuua mkutano huu wote kwa njaa.”

4 dKisha Bwana akamwambia Mose, “Nitanyesha mikate kutoka mbinguni kwa ajili yenu. Watu watatoka kila siku na kukusanya kitakachowatosha kwa siku ile, kwa njia hii, nitawajaribu nione kama watafuata maelekezo yangu. 5 eSiku ya sita watatayarisha kile waletacho ndani, nacho kitakuwa mara mbili kuliko ya kile walichokusanya kila siku.”

6 fKwa hiyo Mose na Aroni wakawaambia Waisraeli wote, “Jioni mtajua kwamba Bwana ndiye aliwatoa Misri, 7 gkisha asubuhi mtauona utukufu wa Bwana, kwa sababu amesikia manungʼuniko yenu dhidi yake. Sisi ni nani hata mtunungʼunikie?” 8 hPia Mose akasema, “Mtajua kuwa alikuwa Bwana wakati atakapowapa nyama mle ifikapo jioni na mikate yote mtakayohitaji asubuhi kwa sababu amesikia manungʼuniko yenu dhidi yake. Sisi ni nani? Hamnungʼuniki dhidi yetu, bali dhidi ya Bwana.”

9Kisha Mose akamwambia Aroni, “Iambie jumuiya yote ya Waisraeli kwamba, ‘Mje mbele zake Bwana, kwa maana amesikia manungʼuniko yenu.’ ”

10 iAroni alipokuwa akizungumza na jumuiya yote ya Waisraeli, wakatazama kuelekea jangwani, na huko wakaona utukufu wa Bwana ukitokeza katika wingu.

11 Bwana akamwambia Mose, 12 j“Nimesikia manungʼuniko ya Waisraeli. Waambie, ‘Jioni mtakula nyama, na asubuhi mtashiba mikate. Ndipo mtajua ya kwamba Mimi ndimi Bwana Mungu wenu.’ ”

13 kJioni ile kware wakaja wakaifunika kambi na asubuhi kulikuwa na tabaka la umande kuzunguka kambi. 14 lWakati umande ulipoondoka, vipande vidogo vidogo kama theluji vilionekana juu ya uso wa jangwa. 15 mWaisraeli walipoona, wakaambiana, “Hiki ni nini?” Kwa kuwa hawakujua kilikuwa kitu gani.

Mose akawaambia, “Huu ndio mkate ambao Bwana amewapa mle.
16Hivi ndivyo Bwana alivyoamuru: ‘Kila mmoja akusanye kiasi anachohitaji. Chukueni pishi
Pishi ni kipimo cha ujazo, kwa Kiebrania ni omeri, ambacho ni sawa na kilo mbili.
moja kwa kila mtu mliye naye katika hema yenu.’ ”

17Waisraeli wakafanya kama walivyoambiwa, baadhi yao wakakusanya zaidi, wengine pungufu. 18 oNao walipopima katika pishi, yule aliyekusanya zaidi hakuwa na ziada, wala aliyekusanya kidogo hakupungukiwa. Kila mmoja alikusanya kiasi alichohitaji.

19 pKisha Mose akawaambia, “Mtu yeyote asibakize chochote mpaka asubuhi.”

20 qHata hivyo, wengine hawakuzingatia aliyosema Mose, wakahifadhi kiasi fulani mpaka asubuhi, lakini kile alichohifadhi kikajaa mabuu na kuanza kunuka. Kwa hiyo Mose akawakasirikia.

21Kila asubuhi, kila mmoja alikusanya kiasi alichohitaji na jua lilipokuwa kali, iliyeyuka. 22 rSiku ya sita, wakakusanya mara mbili, kiasi cha pishi mbili kwa kila mtu, nao viongozi wa jumuiya wakaja kumwarifu Mose. 23 sMose akawaambia, “Hivi ndivyo alivyoagiza Bwana: ‘Kesho itakuwa siku ya mapumziko, Sabato takatifu kwa Bwana. Kwa hiyo okeni kile mnachotaka kuoka na mchemshe kile mnachotaka kuchemsha. Hifadhini chochote kinachobaki na mkiweke mpaka asubuhi.’ ”

24Kwa hiyo wakavihifadhi mpaka asubuhi, kama Mose alivyoagiza, na havikunuka wala kuwa na mabuu. 25Mose akawaambia, “Kuleni leo, kwa sababu leo ni Sabato kwa Bwana. Hamtapata chochote juu ya nchi leo. 26 tKwa siku sita mtakusanya, lakini siku ya saba, yaani Sabato, hakutakuwepo chochote.”

27Hata hivyo, baadhi ya watu wakatoka kwenda kukusanya siku ya saba, lakini hawakupata chochote. 28 uNdipo Bwana akamwambia Mose, “Je, mtaacha kushika maagizo na maelekezo yangu mpaka lini? 29Fahamuni kuwa Bwana amewapa ninyi Sabato, ndiyo sababu katika siku ya sita amewapa mikate ya siku mbili. Kila mmoja inampasa kukaa pale alipo katika siku ya saba. Hata mmoja haruhusiwi kutoka.” 30Kwa hiyo watu wakapumzika siku ya saba.

31Watu wa Israeli wakaita ile mikate mana
Mana maana yake ni mkate kutoka mbinguni.
Ilikuwa myeupe kama mbegu za mtama na ladha yake ilikuwa kama mkate mwembamba uliotengenezwa kwa asali.
32Mose akasema, “Hivi ndivyo alivyoagiza Bwana: ‘Chukueni pishi ya mana na kuhifadhi kwa ajili ya vizazi vijavyo ili vione mikate niliyowapa mle jangwani nilipowatoa katika nchi ya Misri.’ ”

33 wKwa hiyo Mose akamwambia Aroni, “Chukua gudulia na uweke pishi moja ya mana ndani yake. Kisha uweke mbele za Bwana ili kihifadhiwe kwa ajili ya vizazi vijavyo.”

34 xKama Bwana alivyomwagiza Mose, hatimaye Aroni alikuja kuihifadhi ndani ya Sanduku la Ushuhuda. 35 yWaisraeli wakala mana kwa miaka arobaini, mpaka walipofika katika nchi iliyokaliwa na watu; walikula mana hadi walipofika mpakani mwa Kanaani.

36 z(Pishi moja ni sehemu ya kumi ya kipimo cha efa.
Efa moja ni sawa na kilo 22.
)

Copyright information for SwhNEN