‏ Esther 8

Amri Ya Mfalme Kuhusu Wayahudi

1 aSiku ile ile Mfalme Ahasuero akampa Malkia Esta shamba la Hamani, adui wa Wayahudi. Naye Mordekai akaja mbele ya mfalme, kwa kuwa Esta alikuwa amesema jinsi anavyohusiana naye. 2 bMfalme akaivua pete yake ya muhuri, ambayo alikuwa amemnyangʼanya Hamani, akampa Mordekai, naye Esta akamweka Mordekai juu ya shamba la Hamani.

3 cEsta alimsihi tena mfalme, akianguka miguuni pake na kulia. Akamwomba akomeshe mpango mwovu wa Hamani Mwagagi ambao alikuwa ameupanga dhidi ya Wayahudi. 4 dKisha mfalme alimnyooshea Esta fimbo yake ya utawala ya dhahabu naye aliinuka na kusimama mbele yake.

5Esta akasema, “Kama ikimpendeza mfalme, nami kama nikipata kibali naye akiona ni jambo lililo sawa kunitendea na kama akipendezwa nami, basi iandikwe amri ya kuzitangua barua zile Hamani mwana wa Hamedatha, Mwagagi, alizotunga na kuandika kuangamiza Wayahudi katika majimbo yote ya mfalme. 6Kwa maana nitawezaje kuvumilia kuona maafa yakiwapata watu wangu? Nitawezaje kuvumilia kuona maangamizi ya jamaa yangu?”

7Mfalme Ahasuero akawajibu Malkia Esta na Mordekai Myahudi, “Kwa sababu Hamani aliwashambulia Wayahudi, nimetoa shamba la Hamani kwa Esta, naye ameangikwa kwenye mti wa kunyongea. 8 eBasi andika amri nyingine kwa jina la mfalme kwa ajili ya Wayahudi kama unavyoona vyema, kisha uifunge kwa kutia muhuri kwa pete ya mfalme kwa kuwa hakuna andiko lililoandikwa kwa jina la mfalme na kutiwa muhuri kwa pete ya mfalme linaloweza kutanguliwa.”

9 fMara moja waandishi wa mfalme wakaitwa kwenye siku ya ishirini na tatu, mwezi wa tatu, ndio mwezi wa Siwani. Wakaandika yote Mordekai aliyoamuru kwa Wayahudi, kwa majemadari, watawala na wakuu wa majimbo 127 kuanzia Bara Hindi mpaka Kushi.
Kushi hapa ina maana ya Ethiopia.
Maagizo haya yaliandikwa kwa maandishi ya kila jimbo na kwa lugha ya kila mtu pia kwa Wayahudi kwa maandishi yao wenyewe na lugha yao.
10Mordekai aliandika nyaraka kwa jina la Mfalme Ahasuero, akazitia muhuri kwa pete ya mfalme na kuzipeleka kwa njia ya matarishi, ambao waliendesha farasi waendao kasi waliozalishwa maalum kwa ajili ya mfalme.

11Waraka wa mfalme uliwaruhusu Wayahudi katika kila mji kuwa na haki ya kukusanyika na kujilinda wenyewe; kuharibu, kuua na kuangamiza jeshi lolote, taifa lolote au jimbo lile litakalowashambulia wao, wake zao, watoto wao na kuteka mali za adui zao. 12Siku ambayo iliwekwa kwa Wayahudi kufanya hili katika majimbo yote ya Mfalme Ahasuero ilikuwa siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, yaani mwezi wa Adari. 13 hNakala ya tangazo ilikuwa itolewe kama sheria katika kila jimbo na iweze kujulikana kwa watu wa kila taifa, ili kwamba Wayahudi wawe tayari siku hiyo kulipiza kisasi kwa adui zao.

14Matarishi, wakiwa wamepanda farasi wa kifalme, walitoka mbio wakichochewa na agizo la mfalme. Tangazo lilitolewa pia katika ngome ya mji wa Shushani.

15 iMordekai akaondoka mbele ya mfalme akiwa amevaa mavazi ya kifalme ya buluu na nyeupe, taji kubwa la dhahabu na joho la zambarau la kitani safi. Na mji wa Shushani ukasherehekea kwa furaha. 16 jKwa maana kwa Wayahudi ulikuwa wakati wa raha na furaha, shangwe na heshima. 17 kKatika kila jimbo na katika kila jiji, popote waraka wa mfalme ulipofika, kulikuwepo furaha na shangwe miongoni mwa Wayahudi, pamoja na karamu na kushangilia. Na watu wengi wa mataifa mengine wakajifanya Wayahudi kwa sababu ya kuwahofu Wayahudi.

Copyright information for SwhNEN