‏ Ecclesiastes 9

Hatima Ya Wote

1 aKwa hiyo niliyatafakari yote haya nikafikia uamuzi kwamba waadilifu na wenye hekima na yale wanayoyafanya yako mikononi mwa Mungu, lakini hakuna mtu ajuaye kama anangojewa na upendo au chuki. 2 bWote wanayo hatima inayofanana, mwadilifu na mwovu, mwema na mbaya, aliye safi na aliye najisi, wale wanaotoa dhabihu na wale wasiotoa.

Kama ilivyo kwa mtu mwema,
ndivyo ilivyo kwa mtu mwenye dhambi;
kama ilivyo kwa wale wanaoapa,
ndivyo ilivyo kwa wale wasioapa.
3 cHuu ni ubaya ulio katika kila kitu kinachotendeka chini ya jua: Mwisho unaofanana huwapata wote. Zaidi ya hayo, mioyo ya watu, imejaa ubaya na kuna wazimu mioyoni mwao wangali hai, hatimaye huungana na waliokufa. 4Yeyote aliye miongoni mwa walio hai analo tumaini, hata mbwa hai ni bora kuliko simba aliyekufa!

5 dKwa maana walio hai wanajua kwamba watakufa,
lakini wafu hawajui chochote,
hawana tuzo zaidi,
hata kumbukumbu yao imesahaulika.
6 eUpendo wao, chuki yao na wivu wao
vimetoweka tangu kitambo,
kamwe hawatakuwa tena na sehemu
katika lolote linalotendeka chini ya jua.
7 fNenda, kula chakula chako kwa furaha, unywe divai yako kwa moyo wa shangwe, kwa maana sasa Mungu anakubali unachofanya. 8 gDaima uvae nguo nyeupe na daima upake kichwa chako mafuta. 9 hFurahia maisha na mke wako, umpendaye, siku zote za maisha ya ubatili uliyopewa na Mungu chini ya jua, siku zote za ubatili. Kwa maana hili ndilo fungu lako katika maisha na katika kazi yako ya taabu chini ya jua. 10 iLolote mkono wako upatalo kufanya, fanya kwa nguvu zako zote, kwa kuwa huko kuzimu, unakokwenda, hakuna kufanya kazi wala mipango wala maarifa wala hekima.

11 jNimeona kitu kingine tena chini ya jua:

Si wenye mbio washindao mashindano
au wenye nguvu washindao vita,
wala si wenye hekima wapatao chakula
au wenye akili nyingi wapatao mali,
wala wenye elimu wapatao upendeleo,
lakini fursa huwapata wote.
12 kZaidi ya hayo, hakuna mwanadamu ajuaye wakati saa yake itakapokuja:

Kama vile samaki wavuliwavyo katika wavu mkatili,
au ndege wanaswavyo kwenye mtego,
vivyo hivyo wanadamu hunaswa na nyakati mbaya
zinazowaangukia bila kutazamia.

Hekima Ni Bora Kuliko Upumbavu

13 lPia niliona chini ya jua mfano huu wa hekima ambao ulinivutia sana: 14Palikuwa na mji mdogo uliokuwa na watu wachache ndani yake. Mfalme mwenye nguvu akainuka dhidi yake, akauzunguka akaweka jeshi kubwa dhidi yake. 15 mKatika mji huo kulikuwepo mtu mmoja maskini lakini mwenye hekima, naye akauokoa ule mji kwa hekima yake. Lakini hakuna aliyemkumbuka yule maskini. 16 nKwa hiyo, nikasema, “Hekima ni bora kuliko nguvu.” Lakini hekima ya maskini imedharauliwa, wala hakuna anayesikiliza maneno yake.

17 oManeno ya utulivu ya mwenye hekima
husikiwa kuliko makelele ya mtawala wa wapumbavu.
18 pHekima ni bora kuliko silaha za vita,
lakini mwenye dhambi mmoja
huharibu mema mengi.
Copyright information for SwhNEN