‏ Deuteronomy 32

1 aSikilizeni, enyi mbingu, nami nitasema;
sikia, ee nchi, maneno ya kinywa changu.
2 bMafundisho yangu na yanyeshe kama mvua,
na maneno yangu na yashuke kama umande,
kama manyunyu juu ya majani mabichi,
kama mvua tele juu ya mimea myororo.

3 cNitalitangaza jina la Bwana.
Naam, sifuni ukuu wa Mungu wetu!
4 dYeye ni Mwamba, kazi zake ni kamilifu,
njia zake zote ni haki.
Mungu mwaminifu ambaye hakosei,
yeye ni mnyofu na mwenye haki.

5 eWamefanya mambo ya upotovu mbele zake;
kwa aibu yao, wao si watoto wake tena,
lakini ni kizazi kilicho kiovu na kilichopotoka.
6 fJe, hii ndiyo njia ya kumlipa Bwana,
enyi watu wajinga na wasio na busara?
Je, yeye siye Baba yenu, Muumba wenu,
aliyewafanya ninyi na kuwaumba?

7 gKumbuka siku za kale;
tafakari vizazi vya zamani vilivyopita.
Uliza baba yako, naye atakuambia,
wazee wako, nao watakueleza.
8 hAliye Juu Sana alipowapa mataifa urithi wao,
alipogawanya wanadamu wote,
aliweka mipaka kwa ajili ya mataifa
sawasawa na hesabu ya wana wa Israeli.
9 iKwa kuwa fungu la Bwana ni watu wake,
Yakobo kura yake ya urithi.

10 jKatika nchi ya jangwa alimkuta,
katika nyika tupu ivumayo upepo.
Alimhifadhi na kumtunza;
akamlinda kama mboni ya jicho lake,
11 kkama tai avurugaye kiota chake,
na kurukaruka juu ya makinda yake,
ambaye hutanda mabawa yake kuwadaka,
na huwachukua kwenye mabawa yake.
12 l Bwana peke yake alimwongoza;
hakuwepo mungu mgeni pamoja naye.

13 mAkamfanya apande sehemu zilizoinuka za nchi,
akamlisha kwa mavuno ya mashamba.
Akamlea kwa asali toka mwambani,
na kwa mafuta kutoka mwamba mgumu,
14 nkwa jibini na maziwa kutoka makundi ya ngʼombe
na kutoka makundi ya mbuzi,
kwa mafuta ya wana-kondoo na mbuzi,
kwa kondoo dume wazuri wa Bashani,
na kwa ngano nzuri.
Ukanywa damu ya zabibu inayotoa povu.

15 oYeshuruni
Yeshuruni maana yake ni Yeye aliye mnyofu, yaani Israeli (ona pia Kum 33:26; Isa 44:2).
alinenepa na kupiga teke;
alikuwa na chakula tele,
akawa mzito na akapendeza sana.
Akamwacha Mungu aliyemuumba,
na kumkataa Mwamba Mwokozi wake.
16 qWakamfanya Mungu kuwa na wivu kwa miungu yao migeni,
na kumkasirisha kwa sanamu zao
za machukizo.
17 rWakatoa dhabihu kwa pepo, ambao si Mungu:
miungu wasiyoijua,
miungu iliyojitokeza siku za karibuni,
miungu ambayo baba zenu hawakuiogopa.
18 sMkamwacha Mwamba, aliyewazaa ninyi;
mkamsahau Mungu aliyewazaa.

19 t Bwana akaona hili, akawakataa,
kwa sababu alikasirishwa
na wanawe na binti zake.
20 uAkasema, “Nitawaficha uso wangu,
nami nione mwisho wao utakuwa nini,
kwa kuwa wao ni kizazi kilichopotoka,
watoto ambao si waaminifu.
21 vWamenifanya niwe na wivu
kwa kile ambacho si mungu,
na kunikasirisha kwa sanamu zao
zisizokuwa na thamani.
Nitawafanya wawaonee wivu wale ambao si taifa.
Nitawafanya wakasirishwe
na taifa lile lisilo na ufahamu.
22 wKwa maana moto umewashwa kwa hasira yangu,
ule uwakao hadi kwenye vina vya mauti.
Utateketeza dunia pamoja na mazao yake,
na kuwasha moto katika misingi ya milima.

23 x“Nitalundika majanga juu yao
na kutumia mishale yangu dhidi yao.
24 yNitatuma njaa kali dhidi yao maradhi mabaya,
yateketezayo na tauni ya kufisha;
nitawapelekea meno makali ya wanyama mwitu,
na sumu ya nyoka wale watambaao mavumbini.
25 zBarabarani upanga utawakosesha watoto;
nyumbani mwao hofu itatawala.
Vijana wao wa kiume na wa kike wataangamia,
pia watoto wachanga na wazee wenye mvi.
26 aaNilisema ningewatawanya
na kufuta kumbukumbu lao
katika mwanadamu.
27 abLakini nilihofia dhihaka za adui,
adui asije akashindwa kuelewa,
na kusema, ‘Mikono yetu imeshinda;
Bwana hakufanya yote haya.’ ”

28 acWao ni taifa lisilo na akili,
hakuna busara ndani yao.
29 adLaiti wangekuwa na hekima wangefahamu hili,
na kutambua mwisho wao utakuwa aje!
30 aeMtu mmoja angewezaje kufukuza elfu moja,
au wawili kufukuza elfu kumi,
kama si kwamba Mwamba wao amewauza,
kama si kwamba Bwana amewaacha?
31 afKwa kuwa mwamba wao si kama Mwamba wetu,
sawasawa na vile adui zetu wanavyokiri.
32 agMzabibu wao unatoka kwenye mzabibu wa Sodoma,
na kutoka kwenye mashamba ya Gomora.
Zabibu zake zimejaa sumu,
na vishada vyake vimejaa uchungu.
33 ahMvinyo wao ni sumu ya nyoka,
sumu yenye kufisha ya swila.

34 ai“Je, hili sikuliweka akiba
na kulifungia kwenye vyumba vyangu vya hazina?
35 ajNi juu yangu kulipiza kisasi; nitalipiza.
Wakati utakapowadia, mguu wao utateleza;
siku yao ya maafa ni karibu,
na maangamizo yao yanawajia haraka.”

36 ak Bwana atawahukumu watu wake,
na kuwahurumia watumishi wake
atakapoona nguvu zao zimekwisha
wala hakuna yeyote aliyebaki,
mtumwa au aliye huru.
37 alAtasema: “Sasa iko wapi miungu yao,
mwamba walioukimbilia,
38 ammiungu wale waliokula mafuta ya dhabihu zao
na kunywa mvinyo wa sadaka zao za vinywaji?
Wainuke basi, wawasaidie!
Wawapeni basi ulinzi!

39 an“Tazama basi, Mimi mwenyewe, Mimi Ndiye!
Hakuna mungu mwingine ila Mimi.
Mimi ninaua na Mimi ninafufua,
Mimi nimejeruhi na Mimi nitaponya,
wala hakuna awezaye kuokoa kutoka mkononi mwangu.
40 aoNinainua mkono wangu kuelekea mbinguni na kusema:
Hakika kama niishivyo milele,
41 apwakati ninapounoa upanga wangu unaometameta
na mkono wangu unapoushika ili kutoa hukumu,
nitalipiza kisasi juu ya adui zangu
na kuwalipiza wale wanaonichukia.
42 aqNitailevya mishale yangu kwa damu,
wakati upanga wangu ukitafuna nyama:
damu ya waliochinjwa pamoja na mateka,
vichwa vya viongozi wa adui.”

43 arFurahini, enyi mataifa, pamoja na watu wake,
kwa kuwa atailipiza damu ya watumishi wake,
atalipiza kisasi juu ya adui zake
na kufanya upatanisho
kwa ajili ya nchi na watu wake.
44 asMose na Yoshua
Yoshua, yaani Yehoshea kwa Kiebrania, maana yake ni Yehova ni Mwokozi.
mwana wa Nuni wakaja, wakanena maneno yote ya wimbo watu wakiwa wanasikia.
45Mose alipomaliza kuyasoma maneno haya yote kwa Israeli wote, 46 auakawaambia, “Yawekeni moyoni maneno yote ambayo nimewatangazia kwa makini siku hii ya leo, ili kwamba mpate kuwaagiza watoto wenu wayatii kwa bidii maneno yote ya sheria hii. 47 avSiyo maneno matupu tu kwenu, bali ni uzima wenu. Kwa hayo mtaishi maisha marefu katika nchi mnayovuka Yordani kuimiliki.”

Mose Aelezwa Kuhusu Kifo Chake

48 awSiku hiyo hiyo Bwana akamwambia Mose, 49 ax“Kwea katika mapangano ya Mlima Abarimu hadi kilima cha Nebo kilichoko Moabu, ngʼambo ya Yeriko, na uitazame Kanaani, nchi ninayowapa Waisraeli kama milki yao wenyewe. 50 ayUtafia kwenye mlima huo unaokwea na kukusanyika pamoja na watu wako, kama ndugu yako Aroni alivyofia juu ya Mlima Hori naye akakusanyika kwa watu wake. 51 azHii ni kwa sababu ninyi wawili mlivunja uaminifu nami mbele ya Waisraeli kwenye maji ya Meriba-Kadeshi katika Jangwa la Sini, na kwa sababu hamkuuinua utakatifu wangu miongoni mwa Waisraeli. 52 baKwa hiyo, utaiona tu nchi kwa mbali; wewe hutaingia nchi ninayowapa watu wa Israeli.”

Copyright information for SwhNEN