‏ Deuteronomy 24

Sheria Kuhusu Ndoa Na Talaka

1 aIkiwa mtu atamwoa mke na akamchukia kwa sababu ya kukosa adabu, naye akamwandikia hati ya talaka, akampa na kumfukuza kutoka nyumbani kwake, 2ikiwa baada ya kuondoka nyumbani kwake atakuwa mke wa mtu mwingine, 3ikiwa mume wake wa pili atachukizwa naye akamwandikia hati ya talaka, akampa na kumfukuza kutoka nyumbani kwake, au kama akifa, 4 bbasi yule mume wake wa kwanza, ambaye alimpa talaka, haruhusiwi kumwoa tena baada ya mwanamke huyo kuwa najisi. Hayo yatakuwa machukizo machoni pa Bwana. Usilete dhambi juu ya nchi ambayo Bwana Mungu wako anakupa kama urithi.

5 cKama mtu ameoa karibuni, kamwe asipelekwe vitani au kupewa wajibu mwingine wowote. Kwa mwaka mmoja atakuwa huru kubaki nyumbani ili amfurahishe mke aliyemwoa.

6 dUsitoe jozi ya mawe ya kusagia, hata ikiwa lile la juu, kuweka rehani kwa ajili ya deni, kwa sababu itakuwa ni kuweka uhai wa mtu kama dhamana.

7 e fKama mtu akikamatwa akiiba yeyote miongoni mwa ndugu zake wa Waisraeli na kumtenda kama mtumwa au akimuuza, mwizi huyo ni lazima auawe. Nawe utaondoa uovu kutoka miongoni mwenu.

8 gPakitokea magonjwa ya ngozi ya kuambukiza, mwe waangalifu sana kufanya sawasawa na maagizo ya makuhani, ambao ni Walawi. Ni lazima mfuate kwa uangalifu yale niliyowaamuru. 9 hKumbukeni kile Bwana Mungu wenu alichomfanyia Miriamu njiani baada ya ninyi kutoka Misri.

10 iUnapomkopesha jirani yako chochote, usiingie nyumbani kwake kutwaa kile anachokitoa kama rehani. 11Ukae nje na umwache huyo mtu uliyemkopesha akuletee hiyo rehani. 12 jIkiwa mtu huyo ni maskini, usiende kulala ukiwa na hiyo rehani yake katika milki yako. 13 kRudisha vazi lake kabla ya machweo ya jua ili apate kulilalia. Kisha atakushukuru na kitaonekana kama kitendo cha haki mbele za Bwana Mungu wako.

14 lUsimwonee mtu maskini na mhitaji ambaye umemwajiri, akiwa ni nduguyo Mwisraeli au mgeni anayeishi katika mojawapo ya miji yenu. 15 mMlipe ujira wake kila siku kabla ya jua kutua, kwa sababu yeye ni maskini na anautegemea ujira huo. La sivyo, anaweza kumlilia Bwana dhidi yako, nawe ukapata hatia ya dhambi.

16 nBaba wasiuawe kwa ajili ya watoto wao, wala watoto wasiuawe kwa ajili ya baba zao; kila mmoja atakufa kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe.

17 oUsipotoshe hukumu ya mgeni au yatima, au kuchukua vazi la mjane kama rehani. 18Kumbukeni kwamba mlikuwa watumwa huko Misri, naye Bwana Mungu wenu akawakomboa kutoka huko. Hii ndiyo sababu ninawaamuru kutenda hili.

19 pUnapovuna shamba lako na ukasahau mganda, usirudi kuuchukua. Acha kwa ajili ya mgeni, yatima na mjane, ili Bwana Mungu wako aweze kukubariki wewe katika kazi zote za mikono yako. 20 qUnapovuna zeituni kutoka miti yako, usirudie matawi mara ya pili. Acha kilichobaki kwa ajili ya mgeni, yatima na mjane. 21Unapochuma zabibu katika shamba lako la mizabibu usirudie tena. Acha zinazobaki kwa ajili ya mgeni, yatima na mjane. 22Kumbuka kwamba mlikuwa watumwa katika nchi ya Misri. Ndiyo sababu ninawaamuru kufanya hili.

Copyright information for SwhNEN