‏ Deuteronomy 1

Amri Ya Kuondoka Mlima Horebu

1 aHaya ni maneno Mose aliyoyasema kwa Israeli yote jangwani mashariki ya Yordani, ambayo iko Araba, inayokabiliana na Sufu, kati ya Parani na Tofeli, Labani, Haserothi na Dizahabu. 2 b(Ni mwendo wa siku kumi na moja kutoka Horebu kwa njia ya Mlima Seiri mpaka Kadesh-Barnea.)

3 cKatika mwaka wa arobaini, siku ya kwanza ya mwezi wa kumi na moja, Mose aliwatangazia Waisraeli yale yote Bwana aliyomwamuru kuwahusu. 4 dHii ilikuwa baada ya kumshinda Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye alitawala Heshboni, na pia huko Edrei alikuwa amemshinda Ogu mfalme wa Bashani, ambaye alitawala huko Ashtarothi. 5 eHuko mashariki ya Yordani katika nchi ya Moabu, Mose alianza kuielezea sheria hii, akisema:

6 f Bwana Mungu wetu alisema nasi huko Horebu, “Mmekaa vya kutosha katika mlima huu. 7 gVunjeni kambi, msonge mbele kuelekea nchi ya vilima ya Waamori; nendeni kwa watu wote ambao ni majirani wa Araba, katika milima, upande wa magharibi chini ya vilima, katika Negebu na kandokando ya pwani, mpaka nchi ya Wakanaani hadi Lebanoni, na kufika mto mkubwa Frati. 8 hTazama, nimewapa ninyi nchi hii. Ingieni mkaimiliki nchi ambayo Bwana aliapa kuwa angaliwapa baba zenu, Abrahamu, Isaki na Yakobo, pamoja na vizazi vyao baada yao.”

Uteuzi Wa Viongozi

(Kutoka 18:13-27)

9 iWakati ule niliwaambia, “Ninyi mmekuwa mzigo mzito sana kwangu kuwachukua peke yangu. 10 jBwana Mungu wenu ameongeza hesabu yenu, hivi kwamba leo ninyi ni wengi kama nyota za angani. 11 kNaye Bwana, Mungu wa baba zenu na awaongeze mara elfu na kuwabariki kama alivyoahidi! 12 lLakini mimi nitawezaje kubeba matatizo yenu, na mizigo yenu, na magomvi yenu peke yangu? 13 mChagueni baadhi ya watu wenye hekima, wenye ufahamu na wanaoheshimika kutoka kila kabila lenu, nami nitawaweka juu yenu.”

14Mlinijibu, “Shauri ulilolitoa ni zuri.”

15 nKwa hiyo niliwachukua wanaume viongozi wa makabila yenu, wenye hekima na wanaoheshimika, nami nikawateua wawe na mamlaka juu yenu kama majemadari wa maelfu, wa mamia, wa hamsini, na wa makumi, na kama maafisa wa makabila. 16 oNami wakati ule nikawaagiza waamuzi wenu: Sikilizeni magomvi kati ya ndugu zenu na mwamue kwa haki, hata kama shauri ni kati ya ndugu wa Kiisraeli, au kati ya mmoja wa ndugu wa Kiisraeli na mgeni. 17 pMsionyeshe upendeleo katika maamuzi; wasikilizeni wote sawasawa, wadogo kwa wakubwa. Msimwogope mtu yeyote, kwa kuwa hukumu ni ya Mungu. Mniletee mimi shauri lolote lililo gumu sana kwenu, nami nitalisikiliza. 18 qNami wakati ule niliwaambia kila kitu ambacho mngefanya.

Wapelelezi Wanatumwa

(Hesabu 13:1-33)

19 rKisha, kama Bwana Mungu wetu alivyotuamuru, tuliondoka kutoka Horebu na kwenda kuelekea nchi ya vilima ya Waamori, kupitia jangwa lile kubwa lote la kutisha, lile mliloliona, nasi tukafika Kadesh-Barnea. 20Kisha niliwaambia, “Mmefika katika nchi ya vilima ya Waamori, ambayo Bwana Mungu wetu anatupa. 21 sTazama, Bwana Mungu wenu amewapa nchi. Pandeni mkaimiliki kama Bwana, Mungu wa baba zenu, alivyowaambia. Msiogope, wala msikate tamaa.”

22 tNdipo ninyi nyote mkanijia na kusema, “Tupeleke watu watutangulie kuipeleleza nchi kwa ajili yetu, na kutuletea taarifa kuhusu njia tutakayopita, na miji tutakayoiendea.”

23 uWazo hilo lilionekana zuri kwangu; kwa hiyo niliwachagua watu wenu kumi na wawili, mwanaume mmoja kutoka kila kabila. 24 vWaliondoka na kukwea katika nchi ya vilima, wakafika katika Bonde la Eshkoli na kuipeleleza. 25 wWakachukua baadhi ya matunda ya nchi, wakatuletea na kutuarifu, “Ni nchi nzuri ambayo Bwana Mungu wetu anatupa.”

Uasi Dhidi Ya Bwana

(Hesabu 14:20-45)

26 xLakini hamkuwa tayari kukwea, mkaasi dhidi ya amri ya Bwana Mungu wenu. 27 yMkanungʼunika ndani ya mahema yenu na kusema, “Bwana anatuchukia, kwa hiyo alitutoa Misri ili kututia mikononi mwa Waamori kutuangamiza. 28 zTwende wapi? Ndugu zetu wametufanya kufa moyo. Wanasema, ‘Watu wa huko wana nguvu zaidi na ni warefu kuliko sisi tulivyo; miji ni mikubwa, yenye kuta zilizofika juu angani. Zaidi ya hayo, tumewaona Waanaki huko.’ ”

29 aaNdipo nikawaambia, “Msihofu, wala msiwaogope. 30 abBwana Mungu wenu anayewatangulia, atawapigania, kama alivyofanya kwa ajili yenu huko Misri, mbele ya macho yenu hasa, 31 acna pia huko jangwani. Huko mliona jinsi Bwana Mungu wenu alivyowachukua, kama baba amchukuavyo mwanawe, katika njia yote mliyoiendea mpaka mkafika mahali hapa.”

32 adPamoja na hili, hamkumtegemea Bwana Mungu wenu, 33 aeambaye aliwatangulia katika safari yenu, kwa moto usiku na kwa wingu mchana, kuwatafutia mahali penu pa kupiga kambi na kuwaonyesha njia mtakayoiendea.

34 afWakati Bwana aliposikia lile mlilosema, alikasirika, akaapa, akasema: 35 ag“Hakuna mtu wa kizazi hiki kiovu atakayeona nchi nzuri niliyoapa kuwapa baba zenu, 36 ahisipokuwa Kalebu mwana wa Yefune. Yeye ataiona, nami nitampa yeye na wazao wake nchi aliyoikanyaga kwa miguu, kwa sababu alimfuata Bwana kwa moyo wote.”

37 aiKwa sababu yenu Bwana pia alinikasirikia mimi, akasema, “Hutaingia hiyo nchi pia. 38 ajLakini msaidizi wako, Yoshua mwana wa Nuni, ataingia. Mtie moyo, kwa sababu atawaongoza Waisraeli kuirithi hiyo nchi. 39 akWale watoto ambao mliwasema wangelichukuliwa mateka, yaani watoto wenu ambao bado hawajui jema na baya, wataingia katika nchi. Nitawapa hiyo nchi, nao wataimiliki. 40 alBali ninyi geukeni, mwondoke kuelekea jangwani kwa kufuata njia ya Bahari ya Shamu.”

41Ndipo mkanijibu, “Tumemtenda Bwana dhambi. Tutakwenda kupigana, kama Bwana Mungu wetu alivyotuamuru.” Hivyo kila mmoja wenu akachukua silaha zake, huku mkifikiri kuwa ni rahisi kukwea katika nchi ya vilima.

42 amLakini Bwana aliniambia, “Waambie, ‘Msipande kupigana, kwa sababu sitakuwa pamoja nanyi. Mtashindwa na adui zenu.’ ”

43 anHivyo niliwaambia, lakini hamkutaka kusikia. Mliasi dhidi ya amri ya Bwana, na katika kiburi chenu mlienda katika nchi ya vilima. 44 aoWaamori ambao waliishi katika vilima hivyo waliinuka dhidi yenu, wakawafukuza kama kundi la nyuki wakiwapiga njia yote ya Seiri mpaka Horma. 45 apMlirudi na kulia mbele za Bwana, lakini Mungu hakusikiliza kilio chenu, wala hakuwajali. 46 aqHivyo mlikaa Kadeshi kwa siku nyingi, kwa muda ule wote mliokaa huko.

Copyright information for SwhNEN