‏ Amos 8

Maono Ya Nne: Kikapu Cha Matunda Yaliyoiva

1Hili ndilo alilonionyesha Bwana Mwenyezi katika maono: kikapu cha matunda yaliyoiva. 2 aAkaniuliza, “Amosi, unaona nini?”

Nikajibu, “Kikapu chenye matunda yaliyoiva.”

Ndipo Bwana akaniambia, “Wakati umewadia kwa watu wangu Israeli; sitawahurumia zaidi.”

3 b Bwana Mwenyezi asema, “Katika siku ile, nyimbo katika Hekalu zitageuka kuwa maombolezo. Miili mingi, mingi sana: itatupwa kila mahali! Kimya!”

4 cLisikieni hili, ninyi ambao mnawagandamiza wahitaji,
na kuwaonea maskini wa nchi,
5 dmkisema,

“Ni lini Mwezi Mwandamo utakapopita
ili tupate kuuza nafaka,
na Sabato itakwisha lini
ili tuweze kuuza ngano?”
Mkipunguza vipimo,
na kuongeza bei,
na kudanganya kwa mizani zisizo sawa,
6 emkiwanunua maskini kwa fedha,
na wahitaji kwa jozi ya viatu,
na mkiuza hata takataka za ngano
pamoja na ngano.
7 f Bwana ameapa kwake mwenyewe, aliye Kiburi cha Yakobo: “Kamwe sitasahau chochote ambacho wamefanya.

8 g“Je, nchi haitatetemeka kwa ajili ya hili,
nao wote waishio ndani mwake hawataomboleza?
Nchi yote itainuka kama Naili;
itapanda na kushuka kama mto wa Misri.
9 h“Katika siku ile,” asema Bwana Mwenyezi,

“Nitalifanya jua litue alasiri na kuifanya dunia
iwe giza wakati wa mchana mwangavu.
10 iNitageuza sikukuu zenu za kidini kuwa maombolezo,
na kuimba kwenu kote kuwe kilio.
Nitawafanya ninyi nyote mvae nguo ya gunia
na kunyoa nywele zenu.
Nitaufanya wakati ule uwe kama wa kuombolezea mwana wa pekee,
na mwisho wake kama siku ya uchungu.

11 j“Siku zinakuja,” asema Bwana Mwenyezi,
“wakati nitakapotuma njaa katika nchi yote:
si njaa ya chakula wala kiu ya maji,
lakini njaa ya kusikia maneno ya Bwana.
12 kWanaume watayumbayumba kutoka bahari hadi bahari
na kutangatanga kutoka kaskazini mpaka mashariki,
wakitafuta neno la Bwana,
lakini hawatalipata.
13 l“Katika siku ile

“wasichana wazuri na vijana wanaume wenye nguvu
watazimia kwa sababu ya kiu.
14Wale waapao kwa aibu ya Samaria,
au kusema, ‘Hakika kama miungu yenu iishivyo, ee Dani,’
au ‘Hakika kama mungu wa Beer-Sheba aishivyo’:
wataanguka, wala hawatasimama tena.”
Copyright information for SwhNEN