‏ Amos 7

Maono Ya Kwanza: Nzige

1 aHili ndilo alilonionyesha Bwana Mwenyezi katika maono: Alikuwa anaandaa makundi ya nzige baada ya kuvunwa fungu la mfalme na wakati ule tu mimea ya pili ilipokuwa ikichipua. 2 bWakati nzige walikuwa wamekula mimea yote ya nchi, nililia kwa sauti kuu, “Bwana Mwenyezi, samehe! Je, Yakobo atawezaje kuendelea kuishi? Yeye ni mdogo sana!”

3 cKwa hiyo Bwana akaghairi.

Kisha Bwana akasema, “Hili halitatokea.”

Maono Ya Pili: Moto

4 dHili ndilo Bwana Mwenyezi alilonionyesha katika maono: Bwana Mwenyezi alikuwa akiita hukumu ya moto; nao ulikausha vilindi vikuu, ukateketeza nchi. 5 eNdipo nikalia, “Bwana Mwenyezi, nakusihi, zuia! Je, Yakobo atawezaje kuendelea kuishi? Yeye ni mdogo sana!”

6 fKwa hiyo Bwana akaghairi.

Bwana Mwenyezi akasema, “Hili nalo halitatokea.”

Maono Ya Tatu: Timazi

7Hili ndilo alilonionyesha katika maono: Bwana alikuwa amesimama karibu na ukuta ambao ulikuwa umejengwa kwa timazi, akiwa na uzi wa timazi mkononi mwake. 8 gNaye Bwana akaniuliza, “Je, Amosi unaona nini?”

Nikamjibu, “Uzi wa timazi.”

Kisha Bwana akasema, “Tazama, ninaweka uzi wa timazi miongoni mwa watu wangu Israeli; sitawahurumia tena.

9 h“Mahali pa Isaki pa juu pa kuabudia miungu pataangamizwa,
na mahali patakatifu pa Israeli pa kuabudia pataharibiwa;
kwa upanga wangu nitainuka
dhidi ya nyumba ya Yeroboamu.”

Amosi Na Amazia

10 iKisha Amazia kuhani wa Betheli akatuma ujumbe kwa Yeroboamu mfalme wa Israeli, akisema: “Amosi analeta fitina juu yako katikati ya Israeli. Nchi haiwezi kuvumilia maneno yake yote. 11 jKwa kuwa hili ndilo Amosi analosema:

“ ‘Yeroboamu atakufa kwa upanga,
na kwa hakika Israeli watakwenda uhamishoni,
mbali na nchi yao.’ ”
12 kKisha Amazia akamwambia Amosi, “Nenda zako, ewe mwonaji! Urudi katika nchi ya Yuda. Ujipatie riziki yako huko na kutoa unabii wako. 13 lUsiendelee kutoa unabii katika Betheli, kwa sababu hapa ni mahali pa mfalme pa kuabudia na Hekalu la ufalme huu.”

14 mAmosi akamjibu Amazia, “Mimi sikuwa nabii wala mwana wa nabii, lakini nilikuwa mchungaji wa kondoo na mtunza mikuyu. 15 nLakini Bwana akanitoa kutoka kuchunga kondoo na kuniambia, ‘Nenda, ukawatabirie watu wangu Israeli.’ 16 oSasa basi, sikieni neno la Bwana. Ninyi mnasema,

“ ‘Usitabiri dhidi ya Israeli,
na uache kuhubiri dhidi ya nyumba ya Isaki.’
17 p“Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana:

“ ‘Mke wako atakuwa kahaba mjini,
nao wana wako na binti zako watauawa kwa upanga.
Shamba lako litapimwa na kugawanywa,
na wewe mwenyewe utafia katika nchi ya kipagani.
Nayo Israeli kwa hakika itakwenda uhamishoni,
mbali na nchi yao.’ ”
Copyright information for SwhNEN