‏ 1 Kings 22

Mikaya Anatabiri Dhidi Ya Ahabu

(2 Nyakati 18:2-27)

1Kwa miaka mitatu hapakuwa na vita kati ya Aramu na Israeli. 2Lakini katika mwaka wa tatu Yehoshafati mfalme wa Yuda akashuka kwenda kumwona mfalme wa Israeli. 3 aMfalme wa Israeli alikuwa amewaambia maafisa wake, “Je, hamjui Ramoth-Gileadi ni mali yetu na bado hatufanyi chochote kuirudisha kwetu kutoka kwa mfalme wa Aramu?”

4 bKwa hiyo akamuuliza Yehoshafati, “Je, utakwenda pamoja nami kupigana dhidi ya Ramoth-Gileadi?”

Yehoshafati akamjibu mfalme wa Israeli, “Mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, farasi wangu ni kama farasi wako.”
5 cLakini Yehoshafati pia akamwambia mfalme wa Israeli, “Kwanza tafuta shauri la Bwana.”

6 dKwa hiyo mfalme wa Israeli akawaleta pamoja manabii wanaume wapatao mia nne, akawauliza, “Je, niende vitani dhidi ya Ramoth-Gileadi, au niache?”

Wakajibu, “Naam, nenda, kwa kuwa Bwana ataiweka Ramoth-Gileadi mkononi mwa mfalme.”

7 eLakini Yehoshafati akauliza, “Je, hayuko nabii wa Bwana hapa ambaye tunaweza kumuuliza?”

8 fMfalme wa Israeli akamjibu Yehoshafati, “Bado yupo mtu mmoja ambaye kupitia yeye twaweza kumuuliza shauri la Bwana, lakini namchukia kwa sababu huwa hatabiri jambo lolote jema kunihusu mimi, lakini kila mara hunitabiria mabaya tu. Yeye ni Mikaya mwana wa Imla.”

Yehoshafati akajibu, “Mfalme hapaswi kusema hivyo.”

9Kwa hiyo mfalme wa Israeli akamwita mmoja wa maafisa wake na kusema, “Mlete Mikaya mwana wa Imla mara moja.”

10Wakiwa wamevalia majoho yao ya kifalme, mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wameketi juu ya viti vyao vya kifalme katika sakafu ya kupuria, kwenye ingilio la lango la Samaria, pamoja na manabii wote wakiwa wakitabiri mbele yao. 11 gWakati huu Sedekia mwana wa Kenaana alikuwa ametengeneza pembe za chuma, akatangaza, “Hivi ndivyo Bwana asemavyo, ‘Kwa hizi pembe utawapiga na kuwarudisha Waaramu nyuma mpaka wameangamizwa.’ ”

12Manabii wengine wote walikuwa wanatabiri kitu hicho hicho wakisema, “Ishambulie Ramoth-Gileadi na uwe mshindi. Kwa kuwa Bwana ataitia mkononi mwa mfalme.”

13Mjumbe aliyekuwa amekwenda kumwita Mikaya akamwambia, “Tazama, manabii wote kama mtu mmoja wanatabiri ushindi kwa mfalme. Neno lako na likubaliane na lao, nawe unene mema kuhusu mfalme.”

14 hLakini Mikaya akasema, “Hakika kama Bwana aishivyo, nitamwambia kile tu Bwana atakachoniambia.”

15Alipofika, mfalme akamuuliza, “Mikaya, je, twende vitani dhidi ya Ramoth-Gileadi au niache?”

Akamjibu, “Shambulia na ushinde, kwa kuwa Bwana atawatia mkononi mwa mfalme.”

16Mfalme akamwambia, “Je, ni mara ngapi nitakuapisha ili usiniambie kitu chochote ila kweli tu kwa jina la Bwana?”

17 iNdipo Mikaya akajibu, “Niliona Israeli wote wametawanyika vilimani kama kondoo wasio na mchungaji, naye Bwana akasema, ‘Watu hawa hawana bwana. Mwache kila mmoja aende nyumbani kwa amani.’ ”

18Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Sikukuambia kwamba huwa hatabiri jambo lolote jema kunihusu, bali mabaya tu?”

19 jMikaya akaendelea, “Kwa hiyo lisikie neno la Bwana: Nilimwona Bwana ameketi juu ya kiti chake cha enzi pamoja na jeshi lote la mbinguni likiwa limesimama kumzunguka upande wa kulia na wa kushoto. 20Naye Bwana akasema, ‘Ni nani atakayemshawishi Ahabu ili aishambulie Ramoth-Gileadi na kukiendea kifo chake huko?’

“Mmoja akapendekeza hili na mwingine lile.
21Mwishoni, pepo mchafu akajitokeza, akasimama mbele za Bwana na kusema, ‘Nitamshawishi.’

22 kBwana akauliza, ‘Kwa njia gani?’

“Akasema, ‘Nitakwenda na kuwa roho ya uongo katika vinywa vya manabii wake wote.’

Bwana akasema, ‘Utafanikiwa katika kumshawishi. Nenda ukafanye hivyo.’

23 l“Kwa hiyo sasa Bwana ameweka roho ya kudanganya ndani ya vinywa vya hawa manabii wako wote. Bwana ameamuru maafa kwa ajili yako.”

24Kisha Sedekia mwana wa Kenaana akatoka na kumpiga Mikaya kofi usoni. Akauliza, “Huyo Roho kutoka kwa Bwana alipita njia gani alipotoka kwangu ili kusema nawe?”

25 mMikaya akajibu, “Utagundua siku hiyo utakapokwenda kujificha kwenye chumba cha ndani.”

26Kisha mfalme wa Israeli akaagiza, “Mchukueni na mkamrudishe kwa Amoni mtawala wa mji na kwa Yoashi mwana wa mfalme. 27 nMkaseme, ‘Hivi ndivyo asemavyo mfalme: Mwekeni mtu huyu gerezani na asipewe chochote ila mkate na maji mpaka nitakaporudi salama.’ ”

28 oMikaya akasema, “Kama utarudi salama, basi Bwana hajanena kupitia kwangu.” Kisha akaongeza kusema, “Zingatieni maneno yangu, enyi watu wote!”

Ahabu Auawa Ramoth-Gileadi

(2 Nyakati 18:28-34)

29Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda wakaenda Ramoth-Gileadi. 30 pMfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Nitaingia vitani nikiwa nimejibadilisha, lakini wewe uvae majoho yako ya kifalme.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli akajibadilisha na kwenda vitani.

31 qWakati huu, mfalme wa Aramu alikuwa amewaagiza majemadari thelathini na wawili wa magari ya vita, “Msipigane na yeyote, mdogo au mkubwa, isipokuwa mfalme wa Israeli.” 32Wakati wale majemadari wa magari ya vita walipomwona Yehoshafati wakafikiri, “Hakika huyu ndiye mfalme wa Israeli.” Kwa hiyo wakageuka ili wamshambulie, lakini Yehoshafati akapiga kelele, 33wale majemadari wakaona kwamba hakuwa mfalme wa Israeli, nao wakaacha kumfuatilia.

34 rLakini mtu fulani akavuta upinde pasipo lengo na kumpiga mfalme wa Israeli katikati ya kiungio cha mavazi yake ya chuma. Mfalme akamwambia mwendesha gari lake, “Geuza gari na uniondoe mimi katika mapigano, nimejeruhiwa.” 35Vita vikaendelea mchana kutwa, naye Mfalme Ahabu akategemezwa ndani ya gari kuelekea Waaramu. Damu kutoka kwenye jeraha lake ikachuruzika ndani ya gari na jioni yake akafa. 36Jua lilipokuwa linazama, mbiu ikaenea katika jeshi lote: “Kila mtu aende mjini kwake, na kila mtu shambani kwake!”

37Basi mfalme akafa na akaletwa Samaria, nao wakamzika huko. 38 sWakasafisha lile gari la vita katika bwawa la Samaria (mahali makahaba walipooga), na mbwa wakaramba damu yake, sawasawa na neno la Bwana lilivyokuwa limesema.

39 tKwa matukio mengine ya utawala wa Ahabu, pamoja na yote aliyoyafanya, jumba la kifalme alilojenga na kupambwa kwa pembe za ndovu, nayo miji aliyoijengea maboma, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? 40Ahabu akalala pamoja na baba zake. Naye Ahazia mwanawe akawa mfalme baada yake.

Yehoshafati Mfalme Wa Yuda

(2 Nyakati 20:31–21:1)

41Yehoshafati mwana wa Asa akawa mfalme wa Yuda katika mwaka wa nne wa Ahabu mfalme wa Israeli. 42Yehoshafati alikuwa na umri wa miaka thelathini na mitano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka ishirini na mitano. Jina la mama yake aliitwa Azuba binti Shilhi. 43 uKatika kila jambo alitembea katika njia za Asa baba yake wala hakwenda kinyume chake. Alifanya yaliyo mema machoni pa Bwana. Hata hivyo mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko. 44Yehoshafati pia alikuwa na amani na mfalme wa Israeli.

45Kwa habari ya matukio mengine ya utawala wa Yehoshafati, mafanikio aliyokuwa nayo na uhodari wake katika vita, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? 46 vAliondolea mbali katika nchi mahanithi wa mahali pa kuabudia miungu waliobaki huko hata baada ya utawala wa baba yake Asa. 47 wTangu hapo hapakuwepo na mfalme katika Edomu, naibu ndiye alitawala.

48 xWakati huu Yehoshafati akaunda merikebu nyingi za biashara
Au: za Tarshishi (ona pia 1Fal 10:22; 2Nya 9:21; 20:36; Isa 2:16; 60:9).
ili kwenda Ofiri kuchukua dhahabu, lakini kamwe hazikusafiri, kwa maana zilivunjika huko Esion-Geberi.
49Wakati ule, Ahazia mwana wa Ahabu akamwambia Yehoshafati, “Waache watu wangu wasafiri baharini pamoja na watu wako,” lakini Yehoshafati akakataa.

50Kisha Yehoshafati akalala na baba zake, akazikwa pamoja nao katika mji wa Daudi baba yake. Mwanawe Yehoramu akawa mfalme baada yake.

Ahazia Mfalme Wa Israeli

51Ahazia mwana wa Ahabu akawa mfalme wa Israeli huko Samaria katika mwaka wa kumi na saba wa Yehoshafati mfalme wa Yuda, naye alitawala katika Israeli kwa miaka miwili. 52 zAkafanya maovu machoni mwa Bwana kwa sababu alienenda katika njia za baba yake na mama yake na katika njia za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambaye alisababisha Israeli itende dhambi. 53 aaAlimtumikia na kumwabudu Baali na kumghadhibisha Bwana, Mungu wa Israeli, kama vile baba yake alivyokuwa amefanya.

Copyright information for SwhNEN